Kwa Mujibu wa Shirika la habari la AhlulBayt (a.s) – ABNA – Ayatollah Reza Ramezani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa "Wanahabari wa Vyombo vya Habari wa Ahlul-Bayt (a.s)", uliofanyika leo asubuhi mjini Qom kwa ushiriki wa wanahabari na wasomi kutoka Iran na baadhi ya nchi za Afrika, alitoa salamu za pongezi kwa mnasaba wa Masiku Kumi ya Karamat (The Ten Days of Karamat) na kusema:
"Mkutano huu unaweza kuwa fursa kwa jamii ya wanadamu kufahamu maana halisi ya karama. Karama na uadilifu ni misingi muhimu ya Uislamu."
Ayatollah Ramezani pia aliwashukuru waandaaji wa kikao hiki, hasa shirika la habari la ABNA kwa kuratibu tukio hili, na akaongeza:
"Wanaosimulia fikra ya Ahlul-Bayt (a.s) kupitia vyombo vya habari wana uwezo mkubwa na wa kipekee. Hatua ya kwanza ni kutambua na kufahamiana na uwezo huu. Namuomba Dk. Aghamiri na wenzake katika kituo cha dunia ya mtandaoni kuchukua hatua za kutambua uwezo huu ili kuwe na uwanja wa ushirikiano."
Akiendelea, Katibu Mkuu alisema:
"Uwezo huu umetokana na muujiza wa Qur’an, yaani Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambayo yameleta mabadiliko ya kimataifa. Mapinduzi ya Kiislamu yalisababisha Uislamu kujitokeza kama nguzo kuu mbele ya mfumo wa kibeberu wa dunia. Sifa muhimu zaidi ya Mapinduzi haya ni fikra ya AhlulBayt. Tunaamini kuwa fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu ni miale ya fikra ya AhlulBayt (a.s). Ikiwa fikra hii itaeleweka vizuri na kutambulishwa kwa jamii ya leo na ulimwengu, basi tutashuhudia watu wengi zaidi wakikumbatia fikra hii kila siku. Lakini hili linahitaji maelezo sahihi."
Akaongeza:
"Tunaushuhudia mwamko wa kibinadamu duniani. Kama Waislamu walivyopata mwamko na kufahamu majukumu yao, leo tunashuhudia pia mwamko wa kibinadamu kote ulimwenguni. Matukio ya Gaza yamefanya fikra ya muqawama (mapambano) ivuke mipaka ya kijiografia, hadi watu wa Ulaya na Amerika wanaonyesha hisia na msimamo wao."
Ayatollah Ramezani pia alizungumzia nafasi ya ulimwengu wa mtandaoni (digital) na athari zake:
"Kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu nafasi ya mitandao na athari zake. Ingawa si mtaalamu wa moja kwa moja, lakini kutokana na tafiti na vikao na wataalamu, ninathibitisha kuwa ulimwengu wa mtandaoni unaweza kusimamia dini katika nyanja mbalimbali. Hata hivyo, mara nyingine huonyesha uongo kama ukweli. Mfano, tukio kubwa kama la Arubaini halionyeshwi kwa usahihi, lakini tukitokea watu wachache wakaudhi imani yetu huko Ulaya, dunia nzima hujua."
Akaendelea kusema:
"Wajibu wa vyombo vya habari kwa maana kamili ya neno hili ni kuwasilisha ukweli. Hatupaswi kuvitazama vyombo vya habari na mitandao kwa mtazamo wa Ki_Machiavelli (1). Wamagharibi wanaitumia mitandao kwa ajili ya kueneza nguvu zao, lakini sisi tunapaswa kuitumia kwa mtazamo wa kibinadamu na wa ukweli."
"Leo, jihadi ya habari na mtandao siyo duni kuliko jihadi ya kijeshi au ardhini. Wote waliohudhuria hapa wanajihusisha kwa namna ya jihadi. Tunatumaini kuona matokeo mazuri katika nchi zenu kupitia juhudi za wanaosimulia fikra ya AhlulBayt kwa njia ya vyombo vya habari. Tuna utajiri mkubwa wa maudhui, na utajiri huo unapaswa kuonyeshwa vyema katika mitandao."
Katika hitimisho, alisema:
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) alisema mwishoni mwa hotuba yake: "Katika uwanja wa akili bandia (AI), tunapaswa kufikia kiwango cha uzalishaji wa maudhui kinachokidhi mahitaji yetu. Hakuna maudhui yoyote duniani yanayoweza kulinganishwa na maudhui ya AhlulBayt (a.s). Iwapo tutayawasilisha maudhui haya kwa njia za kuvutia na zenye taathira katika mitandao ya kijamii, basi bila shaka tutashinda katika uwanja huu."
Akaongeza: "Kwa kuzingatia sifa za ustaarabu wa Kiislamu, tunaweza kuwa washindi katika medani za fikra kimataifa. Ili kufanikisha hili, taasisi kama Kituo cha Kitaifa cha Mitandao ya Kijamii zinapaswa kuchukua hatua madhubuti katika kuweka mazingira bora ya kuwasilisha maudhui ya Kiislamu na kidini kwa njia zenye mvuto na hadhi."
Akatilia mkazo: "Tunapaswa kuitambulisha dini ya Uislamu kwa namna iliyo kamili na sahihi, si kwa namna iliyopotoshwa ambayo inawasilishwa na Magharibi. Uislamu wa AhlulBayt unatofautiana kwa kiasi kikubwa na aina za Uislamu zinazotangazwa na Magharibi. Huko Magharibi, baadhi ya watu wanajitahidi kuufuta au kuufanya Uislamu uungane na tamaduni za Magharibi; lakini sisi tunapaswa kuutambulisha Uislamu kwa ukamilifu na kwa asili yake halisi."
(1) Tanbihi: (Inaposemwa: "Mitandao ya kijamii kwa mtizamo wa Machiavellian" inarejelea matumizi ya majukwaa ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii (Social Media and Networks) kwa njia zinazolingana na fikra na kanuni za Machiavellian, ambazo mara nyingi huhusisha upotoshaji, udanganyifu, udhibiti wa kimkakati wa habari na tabia inayozingatia matumizi ya nguvu ya kuminya vyombo vya habari).
Your Comment